
Naanza nudhuma, ndugu sikieni
Na mola karima, nampa shukrani
Eidi yetu njema, katupa mannani
Leo ni furaha, eidi kufikia
Ni siku adhwimu, tumepewa sisi
Ndugu mufahamu, si siku ya nuksi
Tuache haramu, na pia maasi
Leo ni furaha, eidi kufikia
Basi tuchezeni, kama mahabasha
Na tuteremeni, na pia kushasha
Vyakula tuleni, piza matobosha
Leo ni furaha, eidi kufikia
Nyingi tabasamu, usoni zitande
Na pia salamu, ziwe kila pande
Tufanye karamu, watu wajipinde
Leo ni furaha, eidi kufikia
Nguo maridadi, na tuzivaeni
Marashi na udi, tujifukizeni
nzuri zawadi, tuwape wendani
Leo ni furaha, eidi kufikia
Enyi sote waja, tufurahikeni
Tuwape pambaja, wote ikhiwani
‘tapata faraja, na pia amani
Leo ni furaha, eidi kufikia
Wote maskini, pia mayatima
Tuwatendeeni, mengi yalo mema
Wawe furahani, kwenye eidi njema
Mtume hashimu, ‘metuweka wazi
Kuwa ni muhimu, kuunga kizazi
Tushikeni hamu, kwenda Kwa wazazi
Leo ni furaha, eidi kufikia
Na wote aila, tuwatembelee
Na zawadi aula, tuwapelekee
Madua Kwa mola, na tuwaombee
Leo ni furaha, eidi kufikia