MABABA WASO HURUMA

      No Comments on MABABA WASO HURUMA

Nawaza na kuwazua, hadi kichwa kuniuma
Nashindwa na kutambua, mababa waso huruma
Naomba jibu murua, munijibu enyi umma
Baba kuwaacha wana, ni nini kama si dhulma?

Baba kuwaacha wana, ni nini kama si dhulma
Tena alosoma sana, ayua ovu na jema
Na wala huruma hana, wana kumuachia mama
Baba kuwaacha wana, ni nini kama si dhulma?

Mbali mno kasafiri, kaacha wana wachanga
Na wala hana habari, kuwa kaacha majanga
Mama naye kasubiri, mpaka muda ukasonga
Baba kuwaacha wana, ni nini kama si dhulma

Mama kafanya sulubu, kazi zisokuwa zake
Akapata na dharubu, huzuni kawa mwenzake
Baba ywala kababu, hajali watoto wake
Baba kuwaacha wana, ni nini kama si dhulma?

Wengi watamani wana, na nyinyi munawatupa
Munanishangaza sana, hakiwapigi kishipa
Basi halali subuhana, mutakuja kuyalipa
Baba kuwaacha wana, ni nini kama si dhulma?

Ni chuki munatutia, na kututoa imani
saa nyingine tunalia, na tunaumia ndani
Mutakuja kujutia, rudini nyuma jamani
Baba kuwaacha wana, ni ni kama si dhulma?

Wengine ni matajiri, na wenye nafasi zao
Wanaishi Kwa sururi, wanaponda mali zao
Ila waona usiri, kutizama wana wao
Baba kuwaacha wana, ni nini kama si dhulma?

Japokuwa masikini, huna mbele wala nyuma
Angaa kuwa na imani, na moyo wenye huruma
Siwaache abadani, watoto wako kinyama
Baba kuwaacha wana, ni nini kama si dhulma?

Nimefikia hatima, ingawa nina hasira
Mababa muso huruma, wallahi munanikera
Acheni basi dhuluma, musije pata hasara
Baba kuwaacha wana, ni nini kama si dhulma?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *