
Sikatai ni ruhusa, kuoa mke wa pili
Basi sifanye mikasa, ukatenda udhalili
Mkeo kumnyanyasa, uadilifu muhali
‘kioa mke wa pili, tenda na uadilifu
‘Sijitie hamnazo, kuoa mke wa pili
Senti usizo nazo, na wala hilo hujali
Ukamfanyia bezo, mke wako wa awali
‘kioa mke wa pili, tenda na uadilifu
Majukumu ‘kakushinda, mke ukamdhulumu
Ukashindwa kujipinda, kumpa vitu muhimu
Nayo ya ndoa matunda, yakawa tena si tamu
‘kioa mke wa pili, tenda na uadilifu
Ametwambia mwenyezi, katika kitabu chake
Ukihofia huezi, ‘sioe wa pili mke
Mke wa Kwanza mpenzi, baki naye peke yake
‘kioa mke wa pili, tenda na uadilifu
Hata kama wajiweza, mali nyingi ja siafu
Zingatia ya muweza, utende uadilifu
Tenda bila ya kusaza, mmoja ‘siwe dhaifu
‘kioa mke wa pili, tenda na uadilifu
Pande moja silemee, ukapeleka zaidi
Kama nyumba wajengee, wote bila ukaidi
Na pia uwapepee, hilo nalo
likibidi
‘kioa mke wa pili, tenda na uadilifu
Nyama ‘kipeleka huku, na upeleke na kule
Si mmoja ala Kuku, na mwengine matembele
Huo ni uzumbukuku, utajibu nini mbele
‘kioa mke wa pili, tenda na uadilifu
Ninakubali mapenzi, hayawezi kufanana
Mmoja ni laazizi, basi atapendwa sana
ili usiweke wazi, mpaka wake wakaona
‘kioa mke wa pili, tenda na uadilifu