Limetutawala zimwi,tena lenye sumu kali
Munalifahamu zimwi?,linalodhoofisha hali
Si lingine ni ukimwi, ugonjwa usiojali
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga
Machozi yatiririka,tena njia mbili mbili
Matumbo yanikatika,kwa ilivyokuwa hali
Sina budi kuandika, kuandika yalo kweli
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga
Ukimwi unasambaa,kama moto wa nyikani
Wanaojiona kung’aa,huingia hatarani
Anasa walozivaa,huwatia mashakani
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga
Ukimwi gonjwa hatari,linatesa na kuua
Linachoma kama nari,ni nani asiyejua
Kwa hiyo ishi vizuri, maisha yalo murua
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga
Unajiona kidume,husikii la mwadhini
Leo upo na mwatime, kesho sijui ni nani
Au ni yule salame,ulomkuta shuleni
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga
Kina binti nanyi pia,tamaa zimewanasa
Maisha mwafurahia,zimewalevya anasa
Mukishaonyeshwa mia,munashindwa kupepesa
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga
Salimu kakupa gari,Ali kakuita hani
Na yule naye omari,kakupeleka saluni
Huo sio ufahari,unajishusha thamani
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga
Ukiwa kichwa kigumu, ukimwi upo njiani
Maisha ‘takuwa sumu,yakutoe furahani
Itakupotea hamu,ya kuishi duniani
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga
Wamezimaliza hela, Kwa madawa kununua
Mwisho wanabaki bila,fikira zawasumbua
Zimewaishia hila,wabaki ‘tungelijua’
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga
Wengine wetu wendani,walelewa na wazazi
Wamebaki vitandani,hawawezi ‘fanya kazi
Na wazazi masikini,wawalea kwa majonzi
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga
Mapenzi kabla ya ndoa,tujaribu kuepuka
Ili gonjwa kuondoa,au japo kupunguka
Na wale waliooa,uaminifu kushika
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga
Jambo moja mufahamu,musilete malumbano
Kuna kusambaza damu, au kudungwa sindano
Kuzijua ni muhimu,njia maarufu mno
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga
Hivyo tuweni makini,kwa njia nilizotaja
Tusijifanyeni duni,tuzindukeni waja
Tuishini kwa amani,tusiikose faraja
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga
Kwa walioathirika,nawapa yangu nasaha
Tamaa ‘sije katika,mukaikosa furaha
Elekeeni kwa rabuka,gonjwa ‘siwape karaha
Ukimwi ni jambo zito,ni zito kushinda nanga