RAFIKI NI MTU GANI?

      2 Comments on RAFIKI NI MTU GANI?

Nawaza na kuwazua, usiku hadi mchana
Ninashindwa kutambua, na kuikosa bayana
Ni jambo lanisumbua, na kuniumiza Sana
Rafiki ni mtu gani? ikhiwani nijibuni

Rafiki alo mzuri, ndiye yupi jamanini
Ni yule aso dosari, akiwa mwako usoni
Ila aiwasha nari, akiondoka machoni
Rafiki ni mtu gani? ikhiwani nijibuni

Au Ni yule sabasi, fitina anazitia
Tena bila wasiwasi, na Moto akachochea
Moyo wake Ni mweusi, hakuna asomjua
Rafiki ni mtu gani? ikhiwani nijibuni

Au yule machachari, mwendani akupotosha
Kisiri na kidhahiri, Moto yeye auwasha
Njia isiyo nzuri, ndiyo anakupitisha
Rafiki ni mtu gani? ikhiwani nijibuni

Ni yupi kweli rafiki, twafaa kumuandama
Asokuwa mnafiki, wala roho ya kinyama
Tena mwenye itifaki, aishi na watu vyema
Rafiki ni mtu gani? ikhiwani nijibuni

Rafiki mwenye kufura, Kama ‘lotiwa hamira
Ni matusi kila Mara, na mwenye nyingi hasira
Kwa huyo rafiki gura, atakutia hasara
Rafiki ni mtu gani? ikhiwani nijibuni

Rafiki hafurahii, wewe ukifanikiwa
Ajifanya hasikii, hata akielezewa
Rafiki namna hii, hafai hata kwa dawa
Rafiki ni mtu gani? Ikhiwani nijibuni

Rafiki alo wa kweli, tena wa kuaminika
Ni yule anokujali, moyoni akakueka
Nazo dua kwa jalali, akuombea hakika
Rafiki Ni mtu gani? ikhiwani nijibuni

2 thoughts on “RAFIKI NI MTU GANI?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *