RAMADHAN YAENDA ZAKE

      No Comments on RAMADHAN YAENDA ZAKE

 

Nipe nguvu ya jalali,nitunge na na kumaliza
Nijaalie sahali, nitunge bila kusaza
Faida zilio aali,waja wote kuwajuza
Ramadhan yaenda zake!

Furaha ilitujaa,kupokea mwezi mwema
Tulijua ni wasaa,wa kuipata salama
Yote yaso manufaa, tukaamua kutema
Ramadhan yaenda zake!

Misikiti ‘lifurika,adinasi furi furi
Pamoja ‘lijumuika,wakati wa kufuturi
Nyoyo zilifuruhika,udugu ukashamiri
Ramadhan yaenda zake!

Wa sigara waraibu, na miraa kadhalika
Kuacha wakajaribu, ibada wakazishika
Mabinti na mashababu, maasi wakaepuka
Ramadhan yaenda zake!

Na kitabu kitukufu, walikisoma kwa shime
Wakasimama kwa safu,ili maovu wazime
Na sehemu zote chafu, zikabakishwa mahame
Ramadhan yaenda zake!

Na wenye kulala Sana, usingizi ‘lipunguza
Wakaziswali za sunna, tena bila mapuuza
Usiku kuamshana, kumuomba mwenye izza
Ramadhan yaenda zake!

Na walio wazinifu, pia walirudi nyuma
Wakashika msahafu,na kutenda yalo mema
Wakayaacha machafu,kwa kungia mwezi mwema
Ramadhan yaenda zake!

Wanaokaa maskani,huko wamekuhujuru
Zimeinuka imani,wameacha kukufuru
‘mekita misikitini,Ni Jambo la kushukuru
Ramadhan yaenda zake!

Ama kweli kwa hakika,mwezi umetuongoza
Tabia ‘mebadilika, ‘metengea walooza
Basi dini kuishika, hata tutapomaliza
Ramadhan yaenda zake!

Kama umebadilika, endelea hivyo hivyo
Na ibada kuzishika,usiende ndivyo sivyo
Na mwezi ‘kikamilika, usiyafanye ya ovyo
Ramadhan yaenda zake!

Mwezi waenda kuisha, ni majonzi si utani
Tumezima tumewasha,tujiulize jamani
Ni vipi zetu bahasha, tumejaza nini ndani?
Ramadhan yaenda zake!

Twakuomba ya jalali,twaomba nasi twalia
Saumu zetu kubali, na ibada zote pia
Na yote yaso halali, ya rabbi tuepushia
Ramadhan yaenda zake!

Naomba hapa kukoma, nimejawa na huzuni
Ramadhan mwezi mwema, waenda fika mwishoni
In shaa Allah mola karima, atufikishe mwakani
Tuuwahi mwezi mwema,salama wa salmini
Farwa mwana wa Halima,jina langu ikhiwani
Ramadhan yaenda zake!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *