MUME DINI NA TABIA

      2 Comments on MUME DINI NA TABIA

‘Likuja mume tajiri, tena mweupe pepepe
Mama kaona fahari, akanioza peupe
Hakuchunguzwa vizuri, kumbe mume ni mapepe
Mengine yote bonasi, mume dini na tabia

Hata awe na majumba, na pesa mpwito mpwito
Ila kidini ayumba, na tabia ni nzito
Huyo si mume ni mamba, ‘takuachia majuto
Mengine yote bonasi, mume dini tabia

Au hizo siksi paksi, na sura ilo jamali
Lakini hayo maasi, afanya bila kujali
Huyo si mume ni nuksi, dadangu tia akili
Mengine yote bonasi, mume dini na tabia

Mtume wetu hashima, ‘metwambia umma wake
kuwa mume alo mwema, ni mwema kwa wake zake
Hivyo basi hima hima, kaka mutanabahike
Mengine yote bonasi, mume dini na tabia

Atapowajia kwenu, mume dini na tabia
Mwozeni mwari wenu, mtume ametwambia
itakuwa bora kwenu, kwani ndiyo sawa ndia
Mengine yote bonasi, mume dini na tabia

2 thoughts on “MUME DINI NA TABIA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *