KUOA MAPEMA

      No Comments on KUOA MAPEMA

Kaka
Naanza wangu usemi, Hoja yangu kutetea
Naikunja yangu ngumi, Uzito kuongezea
Ya kwanza hadi ya kumi, Nyote zitawaelea
Waja kuoa mapema, Kubwa sunna ya Amini

Dada
Basi anza taratibu, ngumi usitukunjie
Wala hakuna sababu, maisha ‘situtishie
Kuwa mstaarabu, tope usiturushie
Ni hatari kubwa mno, wana kuoa mapema

Kaka
Sio jambo la aibu, Shababu kufunga ndoa
Awe na wake muhibu, Ndani kwake akapoa
Na wala sio ajabu, Mapema mja kuoa
Waja kuoa mapema, Kubwa sunna ya Amini

Dada
Nakubali si aibu, ila ni kubwa hatari
Kukurupuka shababu, kuoa pasi hadhari
Atakuja pata tabu, ndoa ikiwaka nari
Ni hatari kubwa mno, wana kuoa mapema

Kaka
Kwanza atasitirika, Kijana atapooa
Maovu tayaepuka, Moyo wake utapoa
Na jicho litafungika, Hata “wakijipodoa”
Waja kuoa mapema, Kubwa sunna ya Amini

Dada
Ndio atasitirika, na maovu mengi sana
pia atafarijika, Kwa kumpata kimwana
Ila atahasirika, ‘kigundua hana mana
Ni hatari kubwa mno, wana kuoa mapema

Kaka
Hasa ni ipi maana, Mja kuishi kapera
Akawa afanya zina, Hamuoni ni hasara
Bora awe na kimwana, Ale wake mshahara
Waja kuoa mapema, Kubwa sunna ya Amini

Dada
Maana hujaijua, ndoa kutoharakisha
Ni kusubiri kukua, akili kumakinisha
Mambo yakawa murua, bila balaa kuzusha
Ni hatari kubwa mno, wana kuoa mapema

Kaka
Kuoa mapema kweli, Kinga bora nakwambia
Ashiki zilizo kali, Ndoani zitatulia
Mesisitiza Rasuli, Vipi unajipingia!!
Waja kuoa mapema, Kubwa sunna ya Amini

Dada
Ni ashiki gani hizi, zilizo kabla ya ndoa
Bwana hakuna mapenzi, kabla mtu kuoa
Ni ibilisi maizi, ataka kukuchomoa
Ni hatari kubwa mno, wana kuoa mapema

Kaka
Mbona hatufikirii, Kilicho haribu umma
Ikawa mbovu jamii,
Mabaya ikayachuma
Ndoa hatushikilii, Mapema natukasoma
Waja kuoa mapema, Kubwa sunna ya Amini

Dada
Usitupake mafuta, Kwa mgongoni mwa chupa
Maovu yakitukuta, chanzo si ndoa hapa
Ni dini kuikamata, na maasi kuyatupa
Ni hatari kubwa mno, wana kuoa mapema

Kaka
Ukichelewa ndoani, Makubwa takukabili
Ipo mingi mitihani, Tabu kustahimili
Kuyafanya ya shetwani, Kwako tawa si muhali
Waja kuoa mapema, Kubwa sunna ya Amini

Dada
Ukiwa na ujasiri, na subira ‘kiishika
Basi maovu na Shari, utaweza kuepuka
Utajipanga vizuri, ndoa kutokurupuka
Ni hatari kubwa mno, wana kuoa mapema

Kaka
Faida zilizotele, Mja mapema kuoa
Akajaitwa mvyele, Heshima akatongoa
Ukapera ni uwele, Leo siri natoboa
Waja kuoa mapema, Kubwa sunna ya Amini

Dada
Ni zipi hizo faida, kama hujamakinika
ila kuna nyingi shida, majukumu kujitwika
Tufanyeni jitihada, ndoa ‘sifanye dhihaka
Ni hatari kubwa mno, wana kuoa mapema

Kaka
Hivi wana wa haramu, Chanzo chao ni kipi?
Na maradhi yalo sumu, Jama yalitoka wapi?
Ni uzinifu qaumu, Japo kwa muda mfupi
Waja kuoa mapema, Kubwa sunna ya Amini

Dada
Chanzo cha wana haramu, ni dini kuipuuza
Na maradhi yalo sumu, ni dini kutotukuza
Ndoa japo ni muhimu, ila tujipange Kwanza
Ni hatari kubwa mno, wana kuoa mapema

Kaka
Mwana akivunja ungo, Hebu na mume apewe
Asije kuwa muongo, Ubikira utolewe
Hivyo tutaziba pengo, Jamii iokolewe
Waja kuoa mapema, Kubwa sunna ya Amini

Dada
Hapo unatupoteza, unisikilize vyema
Mwana utamuumiza, Kwa kumuoza mapema
Ndoa japo ni mwangaza, lakini mwanzo kusoma
Ni hatari kubwa mno, wana kuoa mapema

Kaka
Sitaki kuendelea, Vyema dada nisikiza
Mwanao akipotea, Sije lia na kuwaza
Usia nishakupea, Ni mapema kumuoza
Waja kuoa mapema, Kubwa sunna ya Amini

Dada
Nimekuelewa vyema, hoja zako ni za kweli
Wana kuozwa mapema, ni Jambo lilo aali
Basi tufanyeni hima, maovu ‘situkabili
Ninaunga ni hatari, kuchelewesha kuoa

Wote
Kadi tama tumefika, Usemi twamalizia
Ndoa ni jambo mwafaka, Nadhani metusikia
Basi oeni haraka, Ndugu tunawausia
Nusu ya dini kushika, Ni jambo lilo sawia

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *