
Elimu urithi aali, mwanao kumuachia
Elimu ni kubwa mali, na tena ya kubakia
Elimu bidhaa ghali, katika hii dunia
Elimu wape wanao, tena bila ya kusita
Elimu akiba yao, katu hutokuja juta
Elimu ni kubwa ngao, ya kujilinda na vita
Elimu ndefu safari, basi safiri ‘sichoke
Elimu kubwa bahari, hainayo mwisho wake
Elimu kama ambari, imiliki usifike
Elimu uitafute, kwa ujino na ukucha
Elimu ya pande zote, itafute bila kucha
Elimu usiiate, kukichwa pia kukicha
Elimu wa nazi mti, kochokocho faidaze
Elimu tujizatiti, kuisoma tujikaze
Elimu mgongo uti, basi tusiipuuze
Elimu siyo umri, wana kwa watu wazima
Elimu ya mola amri, basi tufanyeni hima
Elimu ni ufahari, na inakupa heshima
Nafurahia haya shairi sana, ungezichapisha kwa kitabu, ningeyanunua
Asante sana
Shukran zajaakaallah khair
Afwan