DAMU IMEGEUKA MAJI

      No Comments on DAMU IMEGEUKA MAJI

Ninaanza kulitunga, shairi langu jamani
Ni mambo yamenisonga, na kunikaba kooni
Hakika mutaniunga, ‘kiyasoma kwa makini
Bila shaka ni kinaya, damu kugeuka maji

Imegeuka dunia, imani zimetoweka
Ndugu walo halisia, nao ‘megeuka nyoka
Wao kukusaidia, si jambo la uhakika
Bila shaka ni kinaya, damu kugeuka maji

Mapenzi hakuna tena, yale ya mababu zetu
Huko kusaidiana, mandugu hawasubutu
Insi tumefarakana, nyoyo zimejaa kutu
Bila shaka ni kinaya, damu kugeuka maji

Hawapendani mandugu, chuki wameekeana
Kila kuchapo vurugu, na tope kurushiana
Nyoyo zimemea sugu, hazitaki kupatana
Bila shaka ni kinaya, damu kugeuka maji

‘Meturuzuku wadudi, kwa kutupa familia
Ila siye wakaidi, hilo twalipuuzia
Letu kuu uhasidi, hatusafiani nia
Bila shaka ni kinaya, damu kugeuka maji

Wala tusiende mbali, baadhi ya baba zetu
Si kwa hali si kwa mali, wala hawajali katu
Heri wasio ahali, wana imani na utu
Bila shaka ni kinaya, damu kugeuka maji

Mandugu tupendaneni, tuishi kwa itifaki
Kizazi tukiungeni, pia tuacheni chuki
Nyoyo tuzisafisheni, ziwe nyeupe ja chaki
Bila shaka ni kinaya, damu kugeuka maji

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *