YATIMA

      No Comments on YATIMA

Naanza yangu nudhuma
Kwa adabu na heshima
Kumueleza yatima
Hana wa kumtizama

Sio kosa la yatima
Majanga kumuandama
Ni mipango ya karima
Waja wake kutupima

Hufurahika yatima
Akionewa huruma
Hupata kutabasama
Kupendwa na wote umma

Tumpendeni yatima
Kwa kumtendea wema
Ili kwenye pepo njema
Tuweni naye hashima

Unapompa furaha
Wamfariji jeraha
Kwani hilo si mzaha
Ni msiba wa daima

Kuna wengi mayatima
Wanaotamani kusoma
Ila shida darahima
Na pia pa kuegema

Kunao wengine watu
Wasiokuwa na utu
Kuwatesa wasubutu
Bila ya hata huruma

Yatima tusimtese
Wala tusimnyanyase
Kichwani tumpapase
Ndivyo asema hashima

Tusiwaone ni nuksi
Wao ni kama sisi
Tusiweni wabinafsi
Tuishi nao kwa wema

Wengine kwenye jalala
Mahali wanapolala
Na pia chao chakula
Nashindwa hata kusema

Wanakosa matibabu
Maradhi yawaadhibu
Kwa kweli wapata tabu
Hawana wao salama

Wengine wanauawa
Mabinti kunajisiwa
Vile vile wanauzwa
Jamani huu ni unyama

Nauliza langu swali
Kula ya yatima mali
Jamani ni haki kweli?
Tumuogope karima

Malipo ni duniani
Hilo tia maanani
Sijitie matesoni
Kwa kudhulumu yatima

Kesho siku ya hesabu
Pia kunao adhabu
Kwa wanaowapa tabu
Watoto walo yatima

Na hayo yote ni tisa
Kumi ninasisitiza
Yatima kutomliza
Ili tupate salama

Siendelei zaidi
Kukoma inanibidi
Na japo kwenye fuadi
Nina mengi ya kusema

Kikomoni nimefika
Kalamu chini naweka
Jina langu kwa hakika
Farwa shariff mi nasema

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *