
Bisimilahi raufu
Mola ulo mtukufu
Waja wako madhaifu
kwako tunakimbilia
Muumba mbingu na ardhi
Twakuomba yako radhi
Tumeacha ya faradhi
Haramuni twajitia
Ya rabbi twarudi kwako
Hatujui tuendako
Na adhabu zilioko
Latifu tuepushia
Na japo kughafilika
Hiyo Ni yetu huluka
Ila alosalimika
Ni yule anotubia
Haramu aina mbali
Tumezifanya halali
Twafanya bila kujali
Jamani twaangamia
Kwanza huo uzinifu
Na yalo mengi machafu
Twafanya bila ya hofu
Aya twazipuuzia
Mola wetu ya latifu
Kwenye qurani tukufu
Ametaja uzinifu
Katu kutokurubia
Pili Ni huo muziki
Kuuacha hatutaki
Wala hatuoni dhiki
Imani zinafifia
Na jambo lingine tena
Ni urongo twaunena
Hatumchi subhana
Ukweli twaukatalia
Wazazi kuwaheshimu
Pia imekuwa ngumu
Kwa sana twawashutumu
Ni vibaya nawambia
Na lingine Ni uizi
Nao pia ujambazi
Vijana mekosa kazi
Madhambini twajitia
Ni mengi mno maasi
Yametutawala insi
Tumkumbukeni qudusi
Kwake yeye kutubia
Jamani turudi nyuma
Tumuogope karima
Ili kwenye pepo njema
Raufu kuturidhia
Kwa dhati tutubieni
Si dhihaka jamanini
Usiku tusimameni
Ghafuri kumlilia
Tena tutieni nia
Madhambi kutorudia
tatupokea jalia
Na peponi kututia
Nimefikia khatima
Na sina budi kukoma
Ni ipi yangu isima
Farwa shariff nawambia