
Jipinde utavopinda, upatoroke nyumbani
Ujione umeshinda, na ni bingwa duniani
Mwishowe ‘tauma chanda, ungiapo majutoni
tezi na omo mwenenda, marejeo ni ngamani
Maisha yakikushinda, yakakupiga na chini
Mwili wote ukakonda, ukabaki taabani
Maswahibu ‘mekutenda, suluhisho ni nyumbani
Tezi na omo mwenenda, marejeo ni ngamani
Uliyaacha matunda, matamu yenye thamani
‘kashika njia ukenda, kujitia taabuni
Maisha uloyapenda, yamekutoka puani
Tezi na omo mwenenda, marejeo ni ngamani
Uliachiwa uwanda, ukashika usukani
Wazazi ukawavunda, ukaona ni wa nini?
Leo jambi walikunda, wataka rudi nyumbani
Tezi na omo mwenenda, marejeo ni ngamani
Ulikiacha kitanda, kisicho na nukusani
Hima hima ukaenda, kuliko jaa kunguni
Leo mambo ‘mekushinda, nyumbani wakutamani
Tezi na omo mwenenda, marejeo ni ngamani
Hehehe Farwa’s pen. Shairi tamu kweli kweli.
“Hima hima ukaenda, kuliko jaa kunguni”
Asante Sana.
Shairi limegusa mahala pake , limekosha