KABILA KIKWAZO CHA NDOA?

      No Comments on KABILA KIKWAZO CHA NDOA?

 

Kutunga hapa naanza, hisia zangu kutema
Nimeketi na kuwaza, nikakereka mtima
Ni Jambo lanishangaza, wanalolitenda umma
Mbona tufanye kabila, liwe kikwazo cha ndoa?

Aliyeanzisha nani, fikira hini potofu
Eti kabila Fulani, kuwaoa wana hofu
Kila kabila jueni, ameliumba raufu
Kwanini sasa kabila, liwe kikwazo cha ndoa?

‘metuumba subuhana, makabila mbali mbali
Lengo si kubaguana, eti tujione aali
Dhamira ni kujuana, amri yake jalali
Mbona tufanye kabila, liwe kikwazo cha ndoa?

Mume amewajieni, mwenye dini na tabia
Ila hapewi idhini, mke kujichukulia
Kisa kabila jamani, sio haki nawambia
Mbona tufanye kabila, liwe kikwazo cha ndoa?

Akaja mume wa pili, dini hajakumbatia
Ila kabila ni ‘aali’, mke mukampatia
Nauliza langu swali, jama hiyo ndo Sheria?
Mbona tufanye kabila, liwe kikwazo cha ndoa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *