BABA AU MAMA

      10 Comments on BABA AU MAMA

Mwana 1
Ndugu yangu vipi hali,natumai u mzima
Namshukuru jalali, kwani mi nipo salama
Ila nina langu swali,linanikera mtima
Kati ya baba na mama,yupi mwenye kubwa hadhi?

Mwana 2
Mimi ndugu sina neno, namshukuru wadudi
Ila Kwa yako maneno,yamenigusa fuadi
Nakujibu Kwa mifano,ya mafundisho ya jadi
mbona jibu lipo wazi,mama ana hadhi kubwa

Kwanza Kwa miezi tisa,kakubeba Kwa machungu
Hivyo vingi mno visa,hakukuavya ndu’ yangu
Aliyapata mikasa,hakumkufuru Mungu
Mbona jibu lipo wazi,mama ana hadhi kubwa

Mwana 1
Hilo sikatai ndugu,himila aliilea
Ila ‘kileta vurugu,baba ndiyo huumia
Mara ywataka njugu, biriani na bajia
Kati ya baba na mama,yupi mwenye kubwa hadhi?

Mwana 2
Ndugu wanifurahisha,Kwa hoja zilo dhaifu
Mama zogo akizusha,hata ‘kitaka barafu
Huwa anasikitisha,kwa mapana na marefu
Mbona jibu lipo wazi,mama ana hadhi kubwa

Mwana 1
Mama humkera baba,ataka vitu vya ghali
Ni vingi wala si haba,na vingine vya muhali
Wala haudhiki baba,huleta bila kujali
Kati ya baba na mama,yupi mwenye kubwa hadhi?

Mwana 2
Nicheke au nilie,hoja finyu za uongo
Nenda ukaulizie,hiyo bei ya udongo
Usinichafue mie,nikaja kupiga gongo
Mbona jibu lipo wazi,mama ana hadhi kubwa

Na ni tisa hayo yote,kumi ni huko kuzaa
Alienda mbio zote,Kwa kusimama na kukaa
Na huo uchungu wote,si mzaha ni balaa
Mbona jibu lipo wazi,mama ana hadhi kubwa

Ndugu utanuna sana,Ila ukweli nasema
Huo uchungu wa mwana,Aujuae ni mama
Shuka mabonde Kwa sana, upande pia milima
Ila jibu lipo wazi,mama ana hadhi kubwa

Mwana 1
Sijanuna swahibia,Nina hoja mpwito mpwito
Hiyo bili fikiria,na gharama za mtoto
Baba atagharamia,si mchezo ni uzito
Kati ya baba na mama,yupi mwenye kubwa hadhi

Ndugu sikiliza hoja,ilo nzito na Kali
Uchungu wa mara moja, angalau ni sahali
Kisha hupata faraja,maisha yakawa aali
Kati ya baba na mama, yupi mwenye kubwa hadhi

Mwana 2
Lahaula ndugu mpenzi,hebu kuwa na haruma
usicheze na mazazi,Kwa ukweli yanauma
Ni roho ya ujambazi,hiyo yako mi nasema
Mbona jibu lipo wazi,mama ana hadhi kubwa

Umesahau naona,kwamba Kuna na malezi
Hawakukosa walonena,kulea kunao kazi
Hivyo fikiria tena,ubongo ueke wazi
Mbona jibu lipo wazi, mama ana hadhi kubwa

Kiwa usiku hulali,anayekesha Ni mama
Baba bila ya kujali,alala akikoroma
Mama hata Kula hali,ahofia una homa
Mbona jibu lipo wazi, mama ana hadhi kubwa

Mwana 1
Wewe wajifanya gwiji,na wa kushindana bingwa
Ila gharama za uji,nazo pesa za maziwa
Upande wako mi siji,baba ndiye wa kuungwa
Kati ya baba na mama,yupi mwenye kubwa hadhi?

Lingine Ni hiyo Karo, shule mwana akianza
huwa inaleta kero,hela zote kumaliza
Na haleti mgogoro,baba kibwebwe hukaza
Kati ya baba na mama, yupi mwenye kubwa hadhi?

Mwana 2
Huna ufikiriacho,Ila pesa na gharama
Hebu yafungue macho,Kwa vizuri kutazama
Faida ni kochokocho,ukimheshimu mama
Mbona jibu lipo wazi,mama ana hadhi kubwa

Twende mafunzo ya dini,mno yamesisitiza
Na hapa kuwa makini,haya tunayoelezwa
Ushindani ni wa nini,na chuki kuieneza
Mbona jibu lipo wazi,mama ana hadhi kubwa

Ni vyema kuwaheshimu, wazazi wote wawili
‘mesisitiza karimu,Kwa hilo tia akili
Kuwatenga ni haramu,liko mbali na halali
Mbona jibu lipo wazi,mama ana hadhi kubwa

Na hata hivyo lakini,mama ‘mepewa daraja
na hakuna walakini,ni tatu wala si moja
Ni amri ya manani, kwetu sisi wake waja
Mbona jibu lipo wazi,mama ana hadhi kubwa

Mwana 1
Ndugu nimekuelewa,tena bila ati ati
Pongezi wafaa kupewa,Kwa sana kujizatiti
Hoja zako ziko sawa,mama ni mgongo uti
Mama daraja tatu,na ya nne ndio ya baba😊

10 thoughts on “BABA AU MAMA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *