AJALI YA NDEGE ILIOTOKEA

      4 Comments on AJALI YA NDEGE ILIOTOKEA

Kwa huzuni naandika, jamani shairi hili
Iwe tutafarajika, na kuipata sahali
Kwa jambo lililotuka, tumekuwa mbaya Hali
Ila mola ‘meandika, kuepuka ni muhali

Baada ya kupokea, zilo nzito habari
Huzuni ilienea, kote kote sio Siri
Ajali ilotokea, wengi imewaathiri
Dua tunawaombea, awarehemu qahari

Twakuomba ya manani, aila wape sahali
Ili hunu mtihani, waweze kuuhimili
Subira iwe moyoni, kufuru ikae mbali
Pia watie peponi, kusubiri jambo hili

Pia izidi imani, yao wote familia
Wajue ni mtihani, waweze kuvumilia
Asiwaghuri shetani, kufuruni kuingia
Ni mipango ya mananni, hakika ‘meqadiria

Walio pata ajali, ilahi waghufiria
Wawe kwenye njema hali, kaburini wakingia
Na wayajibu maswali, bila shida kupitia
Wafunike na kivuli, qiyama kikifikia

Tulobaki twainama, ni lini yetu sanati
Mauti ni ya lazima, tuacheni ati ati
Twakuomba ya karima, yawe sahali mauti
Na ifikapo qiyama, ututie jannati

Ibada tumesahau,anasa twaziandama
Mungu tunamdharau,bila ya kurudi nyuma
Twajifanya kusahau,kama kuna na qiyama
Tuzindukeni wadau, ili tupate salama

4 thoughts on “AJALI YA NDEGE ILIOTOKEA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *