WALIMU NDIYO PEINTI

      No Comments on WALIMU NDIYO PEINTI

Natoa zangu salamu,walimu nisikizeni

Nashika yangu kalamu,nilivyofunzwa zamani
Alinifunza mwalimu,kuishika Kwa makini
Hivyo natunga nudhumu,Kwa furaha ya moyoni
Kama maisha baiti,walimu ndiyo peinti

Chekechea tukianza,hatujui kuandika
Mwalimu anatufunza,jinsi kalamu kushika
Na Tena anatutunza,tusije kuhangaika
Kwa pamoja tunacheza,sote tunafurahika
Kama maisha baiti,walimu ndiyo peinti

Lingine la kushangaza,Ni kubwa yao subira
Mno mi hunipendeza,ilivyo yao busara
Sichoki kuwapongeza,hata milioni mara
insha’Allah mola muweza,’tawazidisha kungara
Kama maisha baiti, walimu ndiyo peinti

Bado tupo chekechea, sehemu ya mitihani
Haja wamejiendea, watoto surualini
wengine wajililia, wataka kwenda nyumbani
Mwalimu huvumilia,hayo yote maskini
Kama maisha baiti,walimu ndiyo peinti

Shule ya msingi pia, walimu hujizatiti
Elimu kutupatia,sayansi na hisabati
Masomo yote sikia,hufunza Kwa mikakati
na bidii wakatia,tupate cha thamani cheti
kama maisha baiti, walimu ndiyo peinti

Mwenendo wenye heshima,tabia nayo nidhamu
Hawakuziacha nyuma,wapenzi wetu walimu
Ila ‘mesimama wima,kutuongoza Kwa hamu
Kwa dhati Mimi nasema, walimu watu muhimu
Kama maisha baiti, walimu ndiyo peinti

Kiendelea Zaidi,huko shule ya upili
Walimu wenye fuadi,mazito kuyahimili
Wanafunzi wakaidi,vilivyo huwakabili
Ili wapate faidi,Kwa elimu ilo aali
Kama maisha baiti, walimu ndiyo peinti

Sitoipata nafuu,lau hapa nitakoma
Walimu chuo kikuu,Ni muhimu mi nasema
Wametufunza makuu,safarini kutokwama
elimu nyanza za juu,kiurahisi twaisoma
Kama maisha baiti, walimu ndiyo peinti

Nao walimu wa dini, kibwebwe wamejifunga
kutufunza Kwa makini,na kututoa ujinga
Elimu yake manani, kuswali nako kufunga
Na mengi yaso kifani,ili tuupate mwanga
Kama maisha baiti, walimu ndiyo peinti

Ni ufunguo elimu,Kwa maisha yalo aali
Hivyo kama si walimu, tungekuwa mbaya hali
Ila maisha matamu, matamu kama asali
Kwa hivyo tuwaheshimu,sote ala kulli hali
Kama maisha baiti, walimu ndiyo peinti

Mwa walimu mikononi,watu wengi ‘mepitia
Mashuhuri duniani,manasi na injinia
Hivi daktari gani,darasani hakungia
wanayo kubwa thamani, walimu nawasifia
kama maisha baiti, walimu ndiyo peinti

Nimeivuka bahari, nikaenda ufuoni
Nimelishuka na gari,nimefika kituoni
Ila naona usiri,kalamu kueka chini
Walimu watu wazuri,’metutoa ujingani
Kama maisha baiti, walimu ndiyo peinti

Japo uzito naona,kitabu changu kufunga
Nina mengi ya kunena,kama tembe za mpunga
Ila muda nauona, umeenda na kusonga
Jina langu waungwana,farwa shariff nilotunga
Kama maisha baiti, walimu ndiyo peinti

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *