UTAMADUNI PWANI

      No Comments on UTAMADUNI PWANI

‘lirudi toka ulaya,nilikokuwa kazini
‘litanda furaha ghaya, kufika tena nyumbani
‘lipokewa kwa kayaya, ‘lipotua uwanjani
Utamaduni wa pwani,huamsha waleleo

Rafiki na familia, ‘lifurika furifuri
Tayari kunipokea, kwa nyimbo na mashairi
Vifijo nderemo pia,kwa Sana vilishamiri
Utamaduni wa pwani, huamsha waleleo

Nilipofika nyumbani,mambo yote ni murua
Miti ya asumini,nayo miti ya vilua
Imepandwa kwa makini, katika wa nyumbani ua
Utamaduni wa pwani, huamsha waleleo

Na ndani nilipongia,harufu zilishadidi
Harufu za kuvutia,Kama vile za waridi
Kwa makini kusikia, kumbe harufu za udi
Utamaduni wa pwani, huamsha waleleo

Niloungoja wakati, hakika uliwasili
Muda wa maakulati,maakulati yalo aali
Za ukwaju sharubati,na ulojazwa nazi wali
utamaduni wa pwani, huamsha waleleo

Kiangalia pembeni,mate yalinidondoka
Vyakula vilisheheni,na samaki wa kupaka
Na vitoweo laini, ‘lipikwa vikapikia
Utamaduni wa pwani, huamsha waleleo

Tulikula kwa pamoja, njaa zetu kushtaki
Katika sinia moja,na tena kwa itifaki
Niliipata faraja,ilo kubwa sidhihaki
Utamaduni wa pwani, huamsha waleleo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *