USIHUZUNIKE

      1 Comment on USIHUZUNIKE

Usihuzunike mja, masaibu ‘kikufika
Na shida zinapokuja, elekea kwa rabuka
Mwisho wa dhiki faraja, kwa hilo ondoa shaka
Usihuzunike mja, masaibu ‘kikufika

Subira ishikilie, moyoni isikutoke
Imani isififie, thawabu ‘zikenda zake
Kufuruni ‘sijitie, vumilia usichoke
Usihuzunike mja, masaibu ‘kikufika

Dunia uionavyo, ni nyumba ya mitihani
Kabiliana vilivyo, usikwame safarini
Mambo ‘kiwa ndivyo sivyo, usiulize mi kwanini?
Usihuzunike mja, masaibu ‘kikufika

Mja usishike tama, ayamu hazifanani
Shida zisikupe homa, ukawa huna amani
Itafika siku njema, utaingia nuruni
Usihuzunike mja, masaibu ‘kikufika

Hakuna yalo marefu, yasiokuwa na ncha
Laili ikiwa ndefu,bila shaka kutakucha
Hivyo iondoe hofu, wala ‘sicheze chakacha
Usihuzunike mja, masaibu ‘kikufika

Wale wahenga wa zama, katu hawakupotosha
Yale walioyasema, ni busara ya kutosha
Mungu hakupi kilema, mwendo akakukosesha
Usihuzunike mja, masaibu ‘kikufika

‘sije jitia kitanzi, kwa maisha yenye tabu
Ndugu yafute machozi,’sikutishe masaibu
Elekea kwa mwenyezi, ‘tafarajika swahibu
Usihuzunike mja,masaibu ‘kikufika

Ina malipo subira,tena yalo mzo mzo
Hivyo ondoa fikira, yasikusonge mawazo
Mungu ‘takupa ujira, kwa shida upitiazo
Usihuzunike mja, masaibu ‘kikufika

Ewe ndugu nifahamu,kuwa nao ujasiri
Kila saa tabasamu,utaipata sururi
Majanga ‘sikupe hamu, ukakufuru qahari
Usihuzunike mja,masaibu ‘kikufika

Maisha ‘kiwa subili, yawe hayatamaniki
Yakajaa na ukali, yawe pia hayanywiki
Jikaze kwa kila hali, zitakuondoka dhiki
Usihuzunike mja,masaibu ‘kikufika

Anayepanga qahari, mambo yote duniani
Zote hizo kheri shari, yote hayo mitihani Haipingiki qadari, hilo tia maanani
Usihuzunike mja,masaibu ‘kikufika.

1 thought on “USIHUZUNIKE

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *