KUTAPAMBAZUKA KWELI?

      15 Comments on KUTAPAMBAZUKA KWELI?

Kwa mwia mrefu sana, nilikuwa nimekimwa ukomo wa kukimwa na maisha duni na ya idhilali tuliyokuwa tukiishi. Maisha yaliyokuwa hayana mbele wala nyuma, hayatamu hayanyamu. Maisha ya kudharauliwa, kunyoshewa vidole na kuchekwa kila tulipopita. Niliishi pamoja na mama yangu, Bi Subira na ndugu zangu wawili, Ayubu na Salama katika mtaa duni wa Borauhai. Naam! Maisha yalikuwa magumu mno yasiotamanika ila hilo halikunikera zaidi kuliko kitendo alichotufanyia baba yetu. Baba msomi aliyejinyakulia shahada zaidi ya kumi katika taasisi tofauti tofauti za kidini. Baba aliyeichambua dini na kuifahamu kuliko kiganja chake cha mkono. Ndiyo, dini aliifahamu. Alijua linalomkera maulana na linalompendeza ila akaamua kujitia hamnazo na kuitelekeza familia yake tena katika hali ngumu ya kimaisha. Jambo hilo liliniachia maswali tumbi nzima katika akili yangu. ‘’Hatukumbuki? Hatutafuti? Hajui tuko hai au tumekufa? Kishipa hakimpigi? Au moyo wake ulitolewa akaekewa jiwe?’’ Niliwaza laili wa nahari lakini wapi! Sikupata majibu ya maswali yangu yaliyokuwa mazito kushinda nanga. Badala yake, chuki na ghamidha zilikita mizizi katika moyo wangu kila nikimkumbuka mtu huyu kakatima asiye na hata sifa moja ya kuitwa baba. Mmh! Eti baba! Chambilecho Ken Walibora, “Baba kwangu lilionekana tu neno lililoingizwa kwenye kamusi kimakosa; Halikuamsha katika moyo wangu hisia zozote za kutamanisha.’’

Awali, maisha yalikuwa matamu kama asali. mapenzi, huruma, itifaki na furaha zilitamalaki kote kote katika nyumba yetu. Mama yangu daima alikuwa na tabasamu usoni ilioashiria kuridhika na maisha yake. Nani asingeridhika na maisha hayo ya kipeponi? Waama! Maisha yalikuwa bulbul. Siku moja, baba yetu, Mzee Sijalikitu aliaga kusafiri kikazi. Hakusafiri tu bali alitokomea kusikojulikana. Wakati huo mama yangu alikuwa na ujauzito wa Salama, mimi nilikuwa na umri wa miaka mitatu na Ayubu ndio mwanzo alikuwa anajifunza kutembea. Siku ziligeuka kuwa miezi, nayo miezi kuwa miaka lakini hakukuwa na dalili za Mzee Sijalikitu kuzuka. Tulidhani pengine mwenzetu kapatikana na shida fulani lakini la! Tulipata habari nyingi kumuhusu kutoka kwa watu tuliowaamini, marafiki zake na hata familia yake. Tulisikia kuwa alionekana uwanja wa ndege katika yiyo hiyo nchi tulipokuwa tukiishi sisi lakini hakuona ulazima wa kuja kutujulia hali. Aidha, tulisikia kutoka kwa familia yake kuwa alirudi kwao Ushelisheli akaoa mke mwingine na kuhamia Uingereza kuanza maisha mapya. Loh! Baba yake mtu kajisahau kuwa aliacha familia huku. Mmh! Alisahau kweli au ni kusudi? Tulimsubiri hadi tukakata tamaa. Huo ukawa ndio mwanzo wa maisha ya tabu na mashaka. Mwanzo wa ngoma ni lele eti! Sote tulifukuzwa shule na mwenye nyumba akatutoa kwenye nyumba yake kwa kukosa kulipa kodi kwa zaidi ya miezi sita. Tulizurura hapa na pale na hatimaye tukapata msamaria mwema aliyetukodisha kijibanda kwa bei ya chini sana katika mtaa wa Borauhai.

Nilizinduka ghafla kutoka kwenye bahari ya luja na kitu cha kwanza nilichoamua kufanya ni kutunga shairi. Hiyo ndiyo iliokuwa njia ilionipa faraja walau kidogo.
Baba kuwaacha wana, nini kama si dhuluma?
Tena alosoma sana, ajua ovu na jema
Na wala huruma hana, wana kumuachia mama

Baba ndiye kiongozi, tena mwenye majukumu
Sijali hajamaizi, kwamba kwake ni muhimu
Kutekeleza malezi, na tena kuwa na hamu

Moyo wangu huniuma, wengine kuita baba
Nimemzoea mama, sijiu kuita baba
Moyo wangu hunichoma, kama n’lodungwa mwiba

“Afua!” Nilisikia mama akiniita punde tu nilipomaliza kutunga shairi.
“Abee mama!” Niliitika huku nikifunga kijitabu changu na kuelekea nje.
“Anza kutoa toa vyombo tusije tukachelewa kama jana.” Alisema mama yangu aliyeonekana mwenye uchovu usiomithilika. Mchana alienda kuuza viazi na sambusa shuleni na jioni ndiyo kama hivi, anauza chapati, maharagwe na ndizi za kiume. Kwa kweli alichoka sana ila hakuwa na budi. Ilibidi ajikakamue ili aweze kulipa kodi ya kibanda chetu, karo ya shule na mahitaji mengine madogo madogo ya kimsingi. Lisilobudi hubidi ebo!

Ilikuwa nadra sana wateja kumiminika mahali hapo. Aghalabu walikuja wawili watatu na vyakula vikabaki vikitutumbulia macho. Wakati mwengine tulikesha hadi saa saba usiku tukitaraji huenda wateja wakatokea. Macho ya mama yaligeuka mekundu kwa kukesha na kurauka bukrata kwaj jina la kutarazaki. Aidha alifanya kibyongo kwa kuinama sana akifanya kazi mchana kutwa usiku kucha. Hali hiyo ilinikata mno maini. “Hivi sisi ni wa kuteseka namna hii wakati baba tunaye ‘anayekula bata’ Uingereza?” Swali hilo liliniregelea kila nilipofikiria hali yetu ya maisha.

Jioni hiyo hali ilikuwa kama kawaida. Wateja walifika kwa uchache sana na miongoni mwao walinunua chakula kwa mkopo. Wengine walikuwa walevi. Walinunua chakula na kutokomea bila kulipa na mama alipojaribu kuwaambia kuhusu malipo walitishia kumpiga. Alibaki tu amesimama kwa unyonge huku machozi yakimdondoka. Niliungulika ndani kwa ndani na moyo kuniuma sana. Mama alijikaza sana asilie mbele yetu ila ulifika wakati mambo yalimfika kooni na machozi kumtirirka asiweze kuyazuia.
“Mama usilie.” Nilijaribu kumfariji huku sauti inatetemeka na machozi kunibubujika jari moja.
“Mama yenu halii. Mama yenu ni jasiri na daima anatabasamu.” Alijibu huku akifuta machozi kisha akaendelea. “Siwezi kukubali ugumu wa maisha uninyakulie furaha yangu. Vile vile, nyinyi wanangu musiruhusu mtu yeyote au hali yoyote iwayeyushie furaha yenu. Nitafurahi mno lau nitawaona kila wakati mukiogelea kwenye bahari ya furaha. Nitajikakamua nihakikishe nalifanikisha hilo.” Alimaliza, akatukumbatia sote watatu na kutubusu kwenye paa la uso. Niliipata amani na faraja ya kipekee.

Taa ya koroboi iliyokuwa ikitupatia mwangaza hafifu ilizimika ghafla. Hata hivyo, mwezi ulikuwa unang’ara na kuhinikiza mwangaza kote kote. Nuru hiyo iliufanya usiku upendeze na kutusahaulisha adha tuliokuwa tukipitia. Huku tukisubiri wateja, mama alitutolea hadithi tamu tamu za kuchekesha na zenye mafunzo. Tulikuwa tumezama kwenye utamu wa hadithi tuliposikia sauti ya muimbaji maarufu, Brother Nassir, kutoka katika redio jiranini.
Moyo elewa dunia, ni nyumba ya mitihani
Kila linalokujia, ni mipango ya manani
Bora ni kuvumilia, faraja iko njiani
Tuliangaliana, tukatabasamu kisha mama akaendelea na hadithi zake. Muda si muda, tulishutuliwa na sauti za watu msikitini wakiswali. Halikuwa jambo la kawaida watu msikitini kuswali mida kama hiyo kama si Ramadhani. Fikira ya kwanza iliyogonga akilini mwangu ni kuwa mwezi umepatwa. Niliangalia samawatini na naam! Dhana yangu ilikuwa sahihi. Mwezi tuliokuwa tukiutumainia kwa mwangaza nao ulipatwa. Ulipatwa takriban wote na giza likashika usukani. Wale wateja wachache tuliokuwa tukiwasubiria nao hawakufika kutokana na kiza kikali. Loh! Leo ni leo. Mwezi uliachiliwa baada ya saa moja na mwangaza ukarudi katika zamu yake. Vyakula havikuwa vimebaki vingi sana. Hivyo basi, tulikusanya virago tukaingia kwenye kijibanda chetu tayari kujipumzisha.

******
Videge viliruka hapa na pale huku vikiimba nyimbo tamu tamu kwa sauti maridhawa kuashiria siku mpya. Jua nalo liliangaza taratibu na kwa madaha kana kwamba linahofia kuwachoma walimwengu kwa miale yake mikali. Niliamka nikawakuta kina Ayubu wamekwishaamka wanajitayarisha kwenda shuleni. Nilijiunga nao. Tulijipangusa pangusa kwa maji machache yaliokuwa yamebaki, tukavaa mararu mararu yetu na kuelekea nje. Tulimkuta mama akipika sambusa na viazi za kuja kuuza shuleni wakati wa mapumziko.
“Shikamoo maa!” Tulimsabahi.
“Marahaba wanangu. Munaenda shule eh!”
“Ndiyo mama. Hata naona tumechelewa.” Nilisema huku nikiangalia jua lilokuwa limekwishachomoza.
Kipindi cha mapumziko shuleni kilifika. Kilikuwa kipindi nilichokipenda kuliko vipindi vyote. Nilitoka nikamkuta nina ameshafika na kina Ayubu wameketi wanafurahikia sambusa moja moja. Tulikaa kwa pamoja huku tukizungumza na kutaniana kwa furaha. Nilitamani kengele ya kurudi darasani isipigwe ili niendelee kufurahikia uwepo wa mama yangu shuleni. Mmh! Lakini kwani kengele itanisikiliza mimi? Ilipigwa na ikatubidi turudi madarasani. Nilimtazama mama yangu kutoka dirishani akiokota karatasi katika ua wa shule kama ilivyokuwa sheria ya shule kwa wauzaji wote. Aliinama huku sura ameikunja kuashira maumivu aliyokuwa akipitia. Nilihisi macho yangu yamekuwa mazito kwa machozi na hatimaye machozi yalidondoka. Nilijaribu kuirudisha akili yangu darasani lakini wapi! Mawazo yangu yalikuwa mbali. Nilimuwaza mama yangu, mwanamke jasiri aliyeamua ala kuli hali kuyabeba mazito ya ulimwengu kwa tabasamu. Mwanamke aliyejitahidi kuhakikisha wanawe wanaishi kama watoto wengine kwa kupata mahitaji ya kimsingi. Mwanamke aliyeamua kuifuta kabisa fikra ya kuwa ufukura ni kikwazo cha kupata elimu. Fikra ya kuwa ni vigumu mno kuwapatia wana elimu bila ya ushirikiano wa baba.
“Afua tupatie kisawe cha neno mama.”
Nilizinduliwa ghafla kutoka katika bahari ya luja na swali la mwalimu.
“Shujaa.” Niliropokwa.
“Afua unaonekana haupo kabisa darasani. Unawaza nini mtoto mdogo? Kuwa makini. Mtihani hauko mbali.” Alifoka mwalimu kwa ghamidha.
“Nisamehe.” Nilinyenyekea.

Jioni ilifika na kila mwanafunzi akashika sabili kuelekea kwao. Wapo waliokuja kuchukuliwa kwa magari ya kifahari. Wapo waliokuja kuchukuliwa na baba zao kwa baiskeli na wapo waliotembea kwa miguu kama sisi. Nilitamani sana lau na sisi tungekuwa na baba ambaye angekuja kutuchukua kila jioni kutoka shuleni.
“Afua najua unachokiwaza!” Nilizinduliwa na sauti ya Ayubu. “Usiwaze sana dada yangu. Kumbuka tunaye mama anayetupenda sana kwa hiyo futa fikra ya kuwa hatuna mtu wa kumuita baba. Mimi hapa nipo, niiteni baba basi.” Tulicheka sote kwa pamoja, tukashikana mikono na kuelekea nyumbani.

Tulirudi nyumbani tukamkuta mama amezama katika lindi la mawazo. Alishtuka ghafla aliposikia tukiingia.
“Shikamoo mama! Uko sawa?” Nilimuuliza mama kwa wasiwasi mwingi sana.
“Marahaba wanangu. Nipo sawa ila kuna kitu ningependa niwaombe ushauri.”
“Enhe! Tueleze basi, unatutia wahaka wanao.”
“Musijali, ni habari njema na huenda ukawa mwanzo wa maisha mapya.”
“Mmh! Habari njema?” Tulisema kwa pamoja huku tukiangaliana kisha kutabasamu na kutega masikio kwa makini zaidi.
“Ndiyo! Habari njema. Nilipokuwa narudi nyumbani kutoka shuleni, nilikutana na swahiba wangu wa kitambo sana. Tuliongea mengi na akaguswa sana na hali yetu. Hivyo basi ameamua kunisaidia.” Alisema mama kwa furaha ya tasa aliyepata pacha. Aliufunga utaji wake vizuri kisha akaendelea. “Anajuana na wakala anayesafirisha watu kwenda kufanya kazi arabuni. Ameniambia kama nipo tayari nimwambie tuanze matayarisho.”
“Mmh! Hiyo ni habari njema mama. Lakini sisi wanao tutabaki na nani?”
“Naona Afua umekuwa mkubwa na akili yako imekomaa kuliko umri wako. Nakuamini sana mwanangu. Naamini unaweza kujiangalia vizuri na kuwashughulikia ndugu zako wadogo. Mimi sipendelei sana kuwaacha peke yenu lakini inabidi wanangu ili na sisi maisha yetu yabadilike.”
“Sawa mama!” Nilisema kwa unyonge.
Hiyo siku kila mmoja alikuwa kanyamaza ji bila kumuongelesha mwenziwe. Majonzi na unyonge ulienea kwenye nyumba. Tulikuwa tumemzoea sana mama yetu laazizi na tulijua kuondoka kwake kungetuachia upweke na huzuni tele.
Siku iliyofuata mama alienda kwa huyo rafiki yake na matayarisho ya safari yakaanza. Baada ya wiki moja kila kitu kilikamilika na mama akasafiri kwenda arabuni. Aliniachia simu ndogo ya mawasiliano.

Ni mwezi sasa tangu mama asafiri na hatujapta taarifa yoyote kumuhusu. Nilijaribu kumpigia simu karibu mara mia moja lakini hapatikani. Nilijaribu kumpigia huyo rafiki yake lakini naye alisema hajui chochote. Wingu la wasiwasi, huzuni na upweke lilifunika maisha yetu na kuziba matumaini kidogo yaliyokuwa yamebaki. Hata hivyo, nilijikakamua kuhakikisha kuwa naendeleza biashara vizuri na vile vile sikosi kuhudhuria shule. Mungu si Athumani. Niliweza kuyatekeleza hayo yote kwa msaada mdogo wa hapa na pale kutoka kwa ndugu zangu katika biashara.
“Afua simu inaita huku.” Aliniita Salama kutoka ndani. Niliingiwa na furaha isiyo kifani nilipogundua ni simu kutoka kwa mama.
“Halo maa! Hujambo? Uko salama? Tumekutamani maa. Mbona ulinyamaza kwa muda mrefu. Kila kitu kiko sawa?” Nilimsalimu na kumfuatizia na msururu wa maswali.
“Afua mimi nipo salama namshukuru Mola.Na nyinyi huko muko salama? Nimewatamani sana wanangu.” Alisema mama kwa sauti ya kinyonge sana.
“Maa sisi tupo salama ila tumekutamani sana. Umetuachia ukiwa na majonzi. Vipi maisha huko?”
“Mwanangu maisha huku ni magumu mno. Hivi ninavyoongea mimi ni mgonjwa sana na wamekataa kunipeleka hospitali na pia wamekataa katakata kunirudisha huko. Nenda kwa yule rafiki yangu umuelezee haya yote. Mwambie afanye ala kuli hali nirejeshwe huko. Nipo chooni ninanyoongea na wewe. Hawaturuhusu simu kwa hiyo simu yangu naificha huku chooni. Siku ukiona kimya sana ujue simu wameichukua.”
Maneno hayo yaliingia ndani ya moyo wangu na kuuvunja vipande vipande. Ghafla nilijisikia kama nusu mfu. Nilichanganyikiwa. Mwili mzima ulinitetemeka na simu ikaanguka chini pu! Nililia kama mtoto mdogo. Sikuamini yaliyokuwa yametokea. Loh! Kitumbua kilikuwa kimeingia mchanga. Tena mchanga mwingi utakaoweza hata kuyavunja meno ya atakayekitafuna.

Baada ya kujituliza, kumakinisha akili yangu na kuvaa ujasiri, nilienda hadi kwa huyo rafiki yake mama na kumjuza yote yaliomsibu mama.
“Aah! Sasa mimi nitakusaidiaje? Sina msaada wowote mimi. Mama yako alienda arabuni kwa hiari. Hakuna aliyemlazimisha.” Alisema mwanamke yule kwa bezo. Maneno yake yalizidi kunitonesha kidonda kilichokuwa na maumivu makali.
“Tuonee huruma tafadhali. Nenda ukazungumze na yule wakala aliyemsafirisha mama muanze mikakati ya kumrudisha.” Nilisema huku nimepiga magoti na machozi kunitiririka mtindo mmoja.
“Hebu usinipigie magoti mie. Aah nyi mafukara muna kero. Munataka kusaidiwa ila msaada hamuuwezi. Hiyo namba ya wakala. Mtafute musuluhishe matatizo yenu.” Alinirushia kikaratasi alichokuwa ameandika namba ya simu na kunibamizia mlango usoni. Nilinyerereka na kuelekea nyumbani huku hasira na huzuni zikipigania nafasi katika hisia zangu.

Punde tu nilipofika nyumbani, nilimpigia huyo wakala na majibu nilioyapata yaliyafufua matumaini yangu yaliokuwa yamekufa na kufukiwa kwenye shimo lenye kina kirefu. Aliniahidi kufanya lolote katika uwezo wake ili kumrejesha mama nyumbani. Ahadi yake haikuwa kaka tupu la yai kwani baada ya wiki mbili za pandashuka mama alirudi nchini japo hali yake ilikuwa imedhoofika sana. Nilitumia akiba yote niliyokuwa nimeweka kumpeleka mamaa hospitali na kutahamaki hatukuwa na hata senti moja. Hata hivyo, hali ya mama iliimarika na furaha na uchangamfu uliokuwa umetoweka ndani ya nyumba ulirudi tena.

Mama alichukua mikopo kutoka kwa majirani na kuanzisha tena biashara zake.

*****
Moyo ulinienda mbio, kijasho kilinitiririka na mwili kunitetema kama mwenye maradhi ya baridi. Ilikuwa siku ya kutangazwa majibu ya mtihani wa mwisho wa shule ya msingi. Wakati ulifika na nikatuma arafa ya kusubiri majibu. Tururu! Arafa iliingia. Lahaula! Nilikuwa nimeanguka kichwa chini miguu juu. Huzuni ilitanda na tamaa ya kuendelea na shule ya upili ilikatika. Mama yangu aliyekuwa na matumaini makubwa juu yangu alionekana kanywea na kuhuzunika si haba. Alikuwa na uhakika kuwa nitapita tu na kwa hiyo hakuwa na wasiwasi sana kuhusu karo kwasababu alijua nitapata wadhamini. Hiyo ndoto ilionekana kuzima ghafla na tuache kupata wadhamini, hata shule yenyewe pia tulijua sitapata tu. Loh! Mtihani mwingine huu.

Barua za kuitwa shule ya upili zilifika ila mimi sikuwa nimeitwa na hata shule moja. Hata hivyo, mama yangu, mwanamke asiyekubali bahari kummeza mzima mzima, alianza safari ya kunitafutia shule. Kila shule tulioenda tulikataliwa na kufukuzwa kwa bezo lakini mama yangu alikataa kata kata kukata tamaa. Tulizunguka mchana kutwa tena kwa miguu kwasabau hatukuwa na pesa za kutosha za kula fakaifa nauli. Baada ya wiki mbili za mahangaiko, tulipata shule moja mpya ya serikali iliyokuwa ndio mwanzo inafunguliwa. Tulipokelewa vizuri na nikapata nafasi katika shule hiyo. Kizaa zaa kilikuja sasa wakati wa kutafuta pesa za karo, sare na vitabu. Shule ya msingi karo haikuwa nyingi vile kwa hiyo mama aliweza kulipa japo kwa shida kiasi lakini karo ya shule ya upili pesa zilikuwa chungu nzima.

Mama alitia bidi maradufu katika biashara zake lakini wapi! Pesa hazikufikia kiwango kilichohitajika. Hatukuwa na budi ila kuanza kiguu na njia kwenda kwa mtajiri kuomba msaada. Tulivumilia jua kali nje ya nyumba za matajiri na mwisho wa siku wengine walitupa nusu ya robo ya pesa zilizohitajika na wengine walitufukuza. Licha ya mateso na manyanyaso yote, mamake nani akate tamaa? Mama alikuwa ameazimia kuwa lazima watoto wake wapate elimu hata kama ni kwa kupigwa na mawimbi makubwa makubwa ya bahari. Safari ya kutafuta basari kwa wabunge na misaada kwa matajiri iliendelea. Tuliposikia kuna mbunge flani anatoa basari tulikwenda mbio kama mshale, tuliposikia kuna tajiri fulani anasaidia sana upande wa karo, tulijepeleka, alhasili lengo letu lilikuwa kupata karo kwa njia yoyote iwayo. Hata nakumbuka siku moja mama yangu alipoenda kwa tajiri flani kuomba msaada, huyo tajiri alimuuliza maswali mengi kuhusu maisha yake na baba watoto wake na baada kumjibu kwa unyenyekevu, huyo tajiri alisema, “Wanawake wengine bwana munapenda sana kuolewa sasa angalia umeachwa na kuachiwa majukumu ya watoto.”
Jambo hilo lilimkera sana mama lakini wakati mwengine alitusimulia na sote tukacheka kwa pamoja.

Siku ya kuanza shule ilifika na kwa bahati nzuri pesa zilikuwa zimetosha za kununua sare, vitabu na kulipa karo ya muhula mmoja. Mihula mengine mambo yalikuwa yale yale ya kutafuta basari za hape na pale na misaada kwa matajiri. Haikutokea hata siku moja niliyofukuzwa shule na pia ndugu zangu walilipiwa karo kwa wakati.

Nilitia bidii ya mchwa masomoni na muhula wa kwanza niliibuka wa kwanza darasani na alama za juu kabisa. Nilifurahi sana na walimu pia hawakuamini kuwa mwanfunzi aliyeingia shule ya upili na alama kidogo kuliko umri wake angeweza kupata alama za juu hivyo. Mama yangu aidha alifurahi mno na kuanza kuona tena mwanga ndani yangu uliokuwa umefifia. Hali hiyo iliendelea hadi kidato cha nne. Nilijinyakulia zawadi karibia zote shuleni na wadhamini mbali mbali walijitolea kunisomesha kwa hiyo mihula michache iliobaki. Mtihani wa mwisho wa kidato cha nne vile vile niluchafua, kama wasemavyo vijana na kuibuka wa kwanza katika mkoa wetu. Si nderemo, vifijo na vigelegele hivyo shuleni mwetu. Nilibebwa juu juu na mama yangu aliona ufahari na kwa mara ya kwanza alijihisi mtu katika watu. Sifa zangu zilizagaa kwa haraka kama moto wa nyika na shule hiyo vilevile ikajipatia sifa kochokocho. Wazazi walipigania kuwapeleka wana wao katika shule hiyo na huo ndio ukawa mwanzo wa shule hiyo kuwa bora mkoani.

Kulitokea mdhamini aliyeahidi kunisomesha chuo kikuu nchini Uingereza mpaka nitakapomaliza. Bila shaka ulikuwa mwanzo mpya na harufu ya maisha mapya na ya mafanikio niliinusia kwa mbali. Dalili ya mvua ni mawingu na mwanzo kokochi mwisho nazi hunena wenye kunena.Hata hivyo, kulihitajika stakabadhi ambazo zingethibitisha kuwa nikienda Uingereza kuna mtu atakayenidhamini kwa upande wa makazi kwasabau hiyo shule haikuwa na mabweni na huyo mdhamini wangu hakuwa mkazi wa Uingereza. Mtihani mpya huu sasa. Mama yangu aliamua kumtafuta baba yangu ili tu atusaidie upande huo wa stakabadhi. Moyo wake ulimuuma sana kufanya hivyo lakini hakuwa na budi. Mama yangu angebaki yule yule tu wa akitaka lake hata akatwe na upanga lazima alipate tu. Mama alienda mbio zote na hatimaye akapata namba za Mzee Sijalikitu. Alimueleza lengo lake na baba mtu akajibu kwa furaha zote kuwa yupo tayari kwa lolote ilimradi mwanawe apate elimu. Mmh! Huo nao tuuiteje? Au maskini katubu na ameamua palipobakia awasaidie wanawe ala kuli hali.

Mikakati yote ilikamilika na siku ya safari ikafika. Nilimuaga mama yangu na ndugu zangu kwa masikitiko mengi ila sikuwa na jinsi na nafasi kama hiyo nisingehatarisha kuipoteza.

Nilifika katika uwanja wa ndege Uingereza. Nilisubiri kwa takriban dakika kumi lakini sikuona dalili za baba yangu aliyeahidi kuja kunichukua uwanjani hapo kutokeza. Nilidhani labda alipatikana na jambo flani na atafika baada ya muda mchache lakini wapi! Nilisubiri kuanzia saa nane mchana nilipowasili hadi saa nne usiku. Niliingiwa na wasiwasi. Nilimpigia simu karibu mara kumi lakini alikuwa hapatikani. Loh! Leo ni leo. Nililala uwanja wa ndege hadi siku ya pili. Nilifikiria sana hatua ya kuchukua lakini sikupata wazo lolote. Ndiyo mara ya kwanza nimefika katika nchi hiyo na sijui yeyote wala sijui mambo yanavyokwenda huko. Nilijikuta nalia tu kama mtoto mdogo.
“Hey lady!” Nilizinduliwa na sauti ya shababu. Niliinua kichwa huku macho yamegeuka mekundu kwa kulia.
“What’s wrong lady? I have been noticing you since yesterday. Are you waiting for somebody?” Aliniuliza kijana yule.
“I have been waiting for someone since yesterday but there is no sign of him coming.’’ Nilijibu huku machozi yakizidi kunibubujika.
“I am Munir. Don’t worry I will help you.” Alijitambulisha ghulamu yule na kuahidi kunisaidia na kunipeleka kwake nikiendelea kufikiria zaidi cha kufanya. Nilifurahi na kumshukuru sana lakini wakati huo huo nilikuwa na wasiwasi kumfuata mtu nisiyemjua.Alionekana kijana mkarimu na mwenye adabu.Mmh! Lakini ya wahenga ni yale yale, vyote ving’aavyo si dhahabu. Hata hivyo, sikuwa na budi ila kumfuata tu na kutawakuli Kwa mola.

Niliishi katika nyumba ya Munir kwa siku mbili na siku ya tatu nikaamua kumpigia baba yangu. Alhamdulilah! Alishika simu ila aliyoyasema yaliitoa kabisa imani kidogo iliyokuwa imebaki kwake.
“Nilirudi Ushelisheli ile siku ndiyo maana sikuweza kuja kukuchukua ila sasa nisharudi Uingereza. Hata hivyo, nina shughuli nyingi sana sidhani kama tutaonana karibuni. Wewe tafuta tafuta mashauri ukodishe nyumba uishi tu. Huku ni Uingereza bwana kila kitu rahisi rahisi.”
Nilikata simu. Sikutaka kuendelea kusikiza maneno ambayo yangeweza hata kunitia maradhi ya moyo. Eti damu nzito kuliko maji! Hii methali kwangu ilikosa maana. Hivi sasa naona tunaishi katika ulimwengu ambapo maji yamekuwa mazito kuliko damu. Mmh! Kinaya.
Niliishi na huyo ajinabii nisiyehusiana naye ndewe wala sikio lakini alinipa heshima zote kama mtoto wa kike. Nilijihisi salama sana kuishi katika nyumba yake. Wasiwasi niliokuwa nao juu yake hapo awali uliyeyuka wote kama barafu kwenye moto. Nilijihisi kama ambaye naishi na mtu niliyejuana naye Kwa miaka na dahari. Alinipa huduma zote nilizozihitajia na kunifanya nisahau yote aliyonifanyia mtu niliyetokamana naye, damu yangu, baba yangu. Bado mutaing’ang’ania methali ya damu nzito kuliko maji?

Baada ya kukosa kabisa matumaini ya msaada kutoka kwa baba yangu, niliamua kumueleza Munir kuhusu lengo langu la kufika Uingereza. Aliahidi kunisaidia kwa njia zote mpaka ahakikishe nimeanza masomo yangu. Karo haikuwa shida kwasababu nilikuwa na mdhamini wangu kwa hiyo mambo yalikuwa rahisi kidogo.
“I will do anything I can to ensure you get admitted to the university. Consider it done, okay?” Alisema Munir, kijana niliyemuona kama malaika niliyeletewa katika maisha yangu. Ama kweli, duniani kuna watu wenye fuadi nyeupe kama theluji. Watu wenye tabia laini kama hariri na wanaojua maana halisi ya utu.

Siku iliyofuata tu, Munir aliacha shughuli zake zote na kunipeleka chuoni. Alimalizana na mambo yote kama ilivyotakikana na wiki iliyofuata nilitakiwa kuanza masomo yangu. Niliwasiliana na watu nyumbani na walifurahika sana kujua kwamba nimepata msaada.
“Mwanangu lakini unamuamini huyo mtu? Dunia imeharibika. Mtu anayekujua au pengine damu yako anaweza kukufanyia unyama seuze ajinabii?” Aliuliza mama yangu Kwa wasiwasi wa kimama.
“Mama usijali. Huyu kijana huku ni mtu mzuri sana. Hata Mimi nilikuwa na wasiwasi hapo awali lakini nimegundua ni mtu mzuri sana.”
“Sawa mwanangu ila jiheshimu uheshimike. Shikana na maadili mema niliyokufunza mwanangu. Usibadilike ukaniangusha mamako.” Aliendelea kusisitiza mama yangu.
Naam! Bila shaka mzazi yeyote angeshikwa na wasiwasi mwingi kujua mwanawe anaishi katika nchi ya kigeni tena na kijana asiye hirimu yake.

Miezi ilisonga, miaka ikapita na hatimaye nilimaliza masomo yangu salama wa salmini bila kupata madhara yeyote kutoka kwa Munir. Kizuri zaidi alinipatia kazi katika kampuni yake. Loh! Sijui nimlipe nini kijana kwa wema wote aliokuwa akinifanyia. Nilitamani nimuangulie mwezi ili kuthibitisha shukurani zangu kwake. Kilichobaki nilimuombea Mungu tu.

Siku hiyo, ni siku ninayoikumbuka kama ninavyolikumbuka jina langu vile. Ilikuwa tarehe kumi na tatu mwezi wa nne. Nilidamka bukrata kama kawaida yangu na kujitayarisha kuelekea kazini. Nilipokuwa nikitoka chumbani, niliiona barua mlangoni. Moyo ulinidunda ghafla. Barua tena? Kunani? Au Munir ashanichoka jamani? Maswali yaligongana kichwani mwangu na kijasho kunitiririka. Nilifungua barua taratibu huku mikono ikinitetemeka. Ilikuwa barua ndefu iliyoandikwa kiingereza bila shaka. Barua iliyojaa hisia za kimapenzi. Barua iliyonigusa moyo na kuuyeyusha. Munir aliomba kufunga pingu za maisha nami. Nilijawa na furaha isiyo kifani. Nani angelikataa kuolewa na kijana mkarimu, adibu, mpole mwenye sifa tumbi nzima kama mchanga wa bahari?

Alifurahika sana nilipompa jibu langu na bila kusita aliomba kumpigia mama yangu simu na kumuomba idhini na pia aje Uingereza ili mikakati ianze. Mama alifurahika sana na kusafiri pamoja na ndugu zangu. Ndoa ilifungwa, sherehe zikafanywa na hatimaye tukawa rasmi mke na mume.

Ni siku mpya. Alfajiri imeingia. Nimekaa kwenye roshani nikifurahikia upepo mwanana huku nimeshika kikombe cha kahawa. Jua linaanza kuchomoza taratibu na hatimaye kunapambazuka. Ndiyo kumepambzuka

15 thoughts on “KUTAPAMBAZUKA KWELI?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *