PAKA WALA WATU

      No Comments on PAKA WALA WATU

Tarehe 13 Agosti 2010 ilikuwa siku ya furaha ghaya kwangu.Ni siku niliyoisubiri kwa raghba ya mkanja kwa siku ayami.Naam! Katu hawakwenda mrama walolonga,mambo ni kangaja huenda yakaja na bila shaka Leo yamekuja.Tena yamekuja kwa kishindo kikuu kilichoibua furaha katika nyoyo za wapendwa wangu.kuolewa Jambo la kheri ebo!

Nyumba ilisheheni nderemo na vigelegele si haba.Watu walifurika furi furi na wengine walizidi kumiminika.kelele za kila aina zilisikika huku na kule zikichanganyika na nyimbo za harusi.mahalati,mashangazi na majirani wote walivaa madera sare yaliyowachukua sawa sawa. walishirikiana bega kwa bega kuhakikisha kuwa mambo yote yanaenda nywee! Ilipofika alasiri mambo yote yalikuwa barabara! Umoja ni nguvu eti!

Muda huo wote mimi nilikuwa chumbani na mpambaji.Mikono yangu ilikuwa ikimetameta kwa heena iliyochorwa kwa ustadi.uso nao usiseme! Nilipojiangalia kiooni tabasamu ilinitoka kwa jinsi nilivyopendeza.ukiona vyaelea vimeundwa.

Tururu! Arafa iliingia katika rununu yangu.Moyo ulinienda mbio na kuyeyuka Kama donge la barafu.ilikuwa arafa ya mume wangu mtarajiwa.Mwanamume mcheshi,mkarimu,mwenye huruma,mwenye mapenzi na mwenye kujali.Japokuwa alikuwa rijali asiyefahamika asili wala fasili yake hilo halikunitia kiwewe.Alikuwa mwanamume aliyeyabadilisha maisha yangu na kuyajaza furaha isiyomithilika kwa hizi siku chache tangu anipose.mmmmh! Kweli alikuwa mwanamume katika sayari ya wanaume.Au ni yale ya wahenga vyote vingaavyo si dhahabu? La! Hapana! Huyu alikuwa tofauti.

Magharibi ilifika na nikah ikafungwa bila pingamizi.Tukawa rasmi mke na mume.wanawake walicheza harusi kwa kuteremea na baada ya hapo mume wangu akanichukua tukaelekea kwake.

Nilipigwa na butwaa nilipofika katika nyumba ya bwana huyo.Lilikuwa jumba la kifahari lenye vyumba kumi na viwili.Vyumba vyote vilikuwa na kufuli isipokuwa kimoja ambacho kilikuwa changu na mume wangu.Hakukuwa na mtu isipokuwa paka wa kila rangi.Niliingiwa na hofu flani moyoni.

“Usishangae mke wangu! Hi yote mali yako.”Alisema yule bwana huku akicheka kicheko cha kutisha.
“mbona jumba kubwa na hakuna anayeishi isipokuwa paka?”Nilimuuliza hali natetemeka hadi ukucha.
“usijali mke wangu! hili jumba ni urithi kutoka kwa baba yangu na hawa paka…..mi napenda paka.”Alinikumbatia nikaipata faraja.

wiki ya Kwanza maisha yalikuwa shwari ya kupendeza.wiki ya pili ilipopiga hodi tu mambo yalianza kwenda shoto.Nilikuwa na hamu na shakawa ya kujua kwanini vyumba vingine vilikuwa na kufuli.Havikuwahi kufunguliwa tangu nifike hapo.usilolijua ni usiku wa giza na kwangu ulikuwa usiku usokucha ila leo niliamua kuukuchisha .

Nilimsubiri mume wangu atoke nikaenda kuchungulia.Loh! niliona kwa mbali mifupa mingi na mafuvu ya vichwa vya binadamu.Hofu ilinivaa!
“uliambiwa usifungue hivyo vyumba ukajitia kichwa kigumu eh.” Nilisikia sauti ila sikuona mtu.
“Ndiyo ni mimi ninayeongea.”Lahaula? ni paka.Mwili ulinisismka,matumbo yakanikatika,kijasho kikanitiririka.

“kafara yako ilikuwa iwe mwezi ujao ila bwana akirudi ntamwambia tuifanye leo.Unaonekana mkaidi sana”
maneno Yale yaliizidisha hofu yangu maradufu.Nifanyeje?
Nilisubiri saa nane ambapo ulikuwa muda wa paka wote kulala nikanyata nyata na kuelekea getini.Niliparaga geti na kupiga mayowe.Bahati ilikuwa upande wangu.Mpita njia alinisikia na kunisaidia kutoka humo ndani.
” Binti! unafanya nini katika hili jumba la paka wala watu?” Aliniuliza msamaria mwema yule.
“Naomba unisaidie nauli nirudi kwetu.” Nililia huku mwili bado wanitetemeka

Nilimsimulia mama yangu kisa kile cha kutisha .Alitamauka hadi ya kutamauka.
“miguu yako imefanya nini mwanangu?” aliniuliza huku macho kayakodoa.Kutahamaki sina vidole vya miguu.sikuligundua jambo hilo nilipokuwa kule.Loh! kumbe walikuwa wameanza kunila kiungo baada ya kiungo bila mimi kutambua.kuanzia hiyo siku maisha yangu yalichukua mkondo tofauti.Nilikataa kata kata kuolewa.Neno ndoa likawa kama jinamizi katika maisha yangu!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *