JINSI YA KUPIKA CHAI MASALA

      No Comments on JINSI YA KUPIKA CHAI MASALA

Chai ni kinywaji kinachopendwa na kuenziwa mno na watu wengi kote ulimwenguni. Wapo ambao kwamba siku ikipita bila ya kupata japo kikombe kimoja cha chai, hawajihisi wapo sawa. Mmojawapo ni shangazi yangu mpendwa. Mnyime vyakula vyote ila usisubutu kumnyima chai😆. Siku anapokuja nyumbani inabidi nimtafutie kikombe kikubwa au hata kopo au pengine jagi haswa kwasababu kikombe hakimtoshi ng’o. Vile vile, miongoni mwa vyombo ambavyo huwezi kuvikosa katika nyumba yeyote chini ya jua, mojawapo ni chupa ya chai. Haya yote ni kudhihirisha kuwa chai imejinyakulia nafasi adhwimu katika nyoyo za wengi.

Naam! Zipo aina nyingi sana za chai. Ipo aina ile iliozoeleka na wengi na ni maarafu san. Walakin ni vizuri sana kujifunza aina nyingine tofauti tofauti ili angalau ubadilishe ladha. Hivyo basi, leo ninawaletea mapishi ya chai masala. Ni chai yenye ladha maridhawa itakayoongeza mapenzi yako ya chai maradufu. Ungana nami tujifunze kwa pamoja.

*MAHITAJI*
☕ Maziwa kikombe 1
☕Maji kikombe 1
☕ Tangawizi nzima iliyopondwa1/4tspn
☕Iliki iliyosagwa 1/4 tspn
☕Mdalasini iliyosagwa 1/4 tspn
☕ Pilipili manga iliyosagwa 1/4tspn
☕ Karafuu takriban 4
☕Majani chai 1tspn
☕ Sukari

*MATAYARISHO*
☕Bandika maji motoni ueke Mdalasini, pilipili manga, karafuu na tangawizi uache ichemke kwa sekunde kadhaa.
☕Ongeza maziwa uache yachemke Kwa sekunde 2 kisha weka majani chai uache ichemke kwa sekunde 10.
☕ Unaweza ukaweka sukari kabisa au ukaweka baadae wakati wa kuandaa.
☕Chai ipo tayari! Andaa Kwa katai, biskuti za tende, au kitafunio chochote utakachopenda.

*MAMBO MUHIMU KUZINGATIA*
☕Tumeweka viungo vichemke na maji kwanza kabla ya kueka maziwa kwasababu huenda vikasababisha maziwa kukatika.
☕1tspn ni kijiko kile kidogo kabisa( kijiko cha chai)
☕Kiasi cha maji itategemea na uzito wa maziwa na pia itategemea na uzito wa chai unaouhitaji. Mimi napendelea Kwa maziwa ya kawaida ya dukani, Kiasi cha maziwa kiwe sawa na kiasi cha maji.

✔ Natumai mumefaidika wapendwa. Kwa maswali na maelezo zaidi mutanipata Instagram@ farwats_kitchen. Aidha kwa mapishi zaidi, nifuateni katika ukurasa wangu wa you tube @farwat’s kitchen.

#farwatskitchen

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *