#IFIKIE WAZAZI_INAZIMA INAWASHA?

      No Comments on #IFIKIE WAZAZI_INAZIMA INAWASHA?

Ifikie wazazi! Msimu uliosambaa katika kila pembe ya nchi na kuzua mijadala mizito.Aidha ni msimu uliowaacha wengi na bumbuazi huku wengine wakipiga mbizi katika bahari ya luja.Naam,msimu huu au hash tegi hii inamanisha nini au madhumumuni yake hasa nini? Lengo lake kuu ni kuwafikishia wazazi picha za wana wao zisizokuwa za kimaadili ili watanabahike na matendo wanayotenda watoto wao wakiwa katika upeo wa macho yao.Aghalabu wazazi huhadaika na mienendo ya wana wao wakiwa ndani ya nyumba.Wasilolifahamu ni kuwa, hawa watoto wanaowaamini na kuwaona wema, wanatenda mambo yasioandikika wala kumtakika wakiwa nje.Loh! Vyote vingaavyo si dhahabu.

Naam! Wanavyodai ni kuwa,wameamua kutumia njia hii ili kuwafundisha adabu watoto waliopotea au walio katika hatari ya kupotea.Ndiyo,tutazisambaza picha zao,watajutia matendo yao,wazazi nao watainuka katika usingizi mzito na kuona hali halisia ya watoto wao.lakini vipi kuhusu heshima ya watoto hawa?Je watakapokuja kujirekebisha,jamii itawakubali? Watakapokwenda kutafuta kazi siku za usoni, watapokelewa? Wazazi nao watazificha wapi nyuso zao kutokana na aibu waliotiwa na watoto wao? Mmh! Bila shaka itakuwa pigo kubwa kwa waathirika.kwa namna hiyo,itakuwa tumeuwasha moto au tumeuzima?Tumezisuka nywele au tumezinyoa?Tumeziba au tumebomoa?

Jambo usilolijua ni usiku wa kiza eti! Tena kiza totoro kinachoweza kusababisha watu kujikwaa au pengine kuhatarisha maisha yao wanaoyathamini.Hivyo basi, ni vyema kumpa mwanga yeyote anayeonekana yupo katika kiza.Naam,#ifikie wazazi imekuja kuwapa mwanga na kuwaamsha wazazi waliolala usingizi mzito.Wazazi ni watu wanaowapenda watoto wao kuliko mtu yeyote yule na aghlabu huwa vigumu mno kuyakubali maovu ya wana wao.kwa sababu hiyo,#ifikie wazazi imeamua kuwaletea thibitisho mbele ya macho yao.Bila Shaka hii Ni njia muafaka itakayowafanya kuamini watake wasitake.

Vile vile, itakuwa funzo kwa wengine walio katika harakati ya kutekeleza uchafu huu.Watakapoiona fedheha walioipata wendani wao bila shaka watachukua hatua nyuma na kujimakinisha.Naam, visa vya aina hiyo vitapungua bila pingmizi.

Mui huwa mwema walilonga! Huenda mbinu hii ikawagusa nyoyo na kuwafanya watubie na warudi kwa muumba wao.Aidha huenda wakabadili mienendo na kuwa na tabia njema ambayo wasingekuwa nayo Lau si kwa mbinu hii.Wapo watu wasiopigika kishipa lau wataelezewa maovu yao uso kwa macho ila watauhisi uovu wa maovu yao lau tu yatadhihirishwa mbele ya watu. kurekebishika kwao huenda kukawafanya wakapigiwa mifano bora siku za usoni.Hivyo basi kuwapa wanaotenda maovu muanga wa kuwa na wao pia si muhali kurekebishika.kutawafanya waliokata tamaa ya kuwa wema kuyatazama maisha kwa mtizamo tofauti.

Katika historia ya kiislamu wapo wengi waliokuwa waovu ila hatimaye walibadilika na kuwa watetezi wakuu wa uislamu.Mfano ni Khalid bin Walid na Umar ibnul khatwab.Maovu yao ya kitambo yalitambulika katika kila pembe ya makka na madina ila walipoukubali uislamu walipokelewa kwa mikono miwili na tabia zao za nyuma kutupiliwa mbali.Hivyo basi maovu ya nyuma yasiwe chanzo Cha mtu kutokubalika na jamii.Wanaosema husema mitandao haisahau.naam,hilo ni kweli kabisa ila kwa wenye busara na hekima, pindi watakapoziona picha hizo watafahamu kuwa ni mambo ya nyuma na maisha Ni tofauti kwao sasa.ila kwa mahasidi na wasiotumia akili zao vilivyo watazikejeli picha hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *