SHUJAA WA MASHUJAA_KHALID BIN WALID

      No Comments on SHUJAA WA MASHUJAA_KHALID BIN WALID

Shujaa ni nani? Je ni yule anayejitia kitanzi kwa ajili ya mpenzi wake? Au yule anayetenda mambo makubwa na maovu ili aonekane mbabe mbele ya wenzake? Pengine yule anayetia watu kabare na kuwadhulumu mali zao? Au yule mwenye mamlaka makubwa na anayeyatumia mamlaka hayo kuwanyanuasa na kuwatesa watu kisha akajinaki kuwa hakuna anayeweza kumpiku? Mmh! Bila shaka hao wako mbali na ushujaa wenyewe.

Wapo mashujaa wengi walioacha historia iliyoandikwa kwa wino usioweza kufutika abadaan kataan kuche kusiche! Kila ninaposikia neno shujaa basi jina linalonijia kwa haraka akilini mwangu ni Khalid bin Walid.Khalid bin Walid! Shababu shupavu,jasiri na shujaa aliyeacha nyayo ndani ya nyoyo za wengi waliomjua na waliomsikia.

Khalid bin Walid ambaye kwamba laqab yake Ni sayfullah alikuwa swahaba wa mtume Muhammad (saw) na kamanda wa jeshi msifika.Alitoka katika kabila la maqureysh ambalo liliwahi kuwa mpinzani mkubwa wa uislamu.Vile vile alitambulika na kusifika sana kutokana na mbinu zake pamoja na ubabe wake katika Vita.Ilikuwa chini ya uongozi wake wa kivita ambapo bara arabu kwa mara ya kwanza katika historia liliunganishwa na khilafa.

Aidha Khalid bin Walid alichangia pakubwa kushindwa kwa waislamu katika vita vya uhud.Ilikuwa nadra Sana watu kushindwa vita wakati yeye ni miongoni mwao.Hata hivyo,alisilimu na kuwa mtetezi mkubwa wa waislamu.vile vile alishiriki katika vita tofauti tofauti pamoja na mtume Muhammad (saw), miongoni mwavyo ikiwa vita vya mutah.

Inasemekana Khalid bin Walid alipigana zaidi ya Vita Mia moja ila hakufa katika vita hivyo bali alifia kitandani.Hata hivyo, hilo halikumfurahisha kwani alikuwa na hamu na shauku ya kufa shahidi ndani ya uwanja wa Vita.Alifurahika sana alipokuwa ndani ya Vita kuliko mahali pengine popote.Alisema, “Ninapokuwa ndani ya uwanja wa vita nafurahikia Sana hata kuliko usiku wangu wa kwanza wa ndoa na msichana mrembo zaidi kuliko wote.” Kutokufa kwake shahidi kulimhuzunisha na kumsononesha sana akasema, “nimepigana vita vingi mno nikiutafuta ushahidi.katika mwili wangu hakuna sehemu isiyokuwa na kovu au kidonda vilivyosababishwa kwa kudungwa mshale na upanga ila leo nafa kitandani Kama ngamia mzee.Macho ya mwoga yasiwahi pumzika.” Mkewe alipoiona huzuni ya mumewe alimwambia, “umepewa laqab ya sayfullah yaani upanga wa Allah na upanga wa Allah hauwezi vunjika.Hivyo Basi,haukujaaliwa kufa Shahidi bali kufa mshindi.

Abubakar aliposikia kuhusu kifo Cha Khalid bin Walid alisema, “Wanawake hawatozaa mfano kama wa Khalid bin walid.”

Ni shujaa wa dunia,kijana huyu jamani
Ni upanga wa jalia,jasiri aso kifani
‘lipigana vita mia,akafia kitandani
Japokuwa yake Nia,ni kufia uwanjani
Ila haikutimia,nia yake masikini
Mkewe akamwambia,isikutande huzuni
Ni mipango ya jalia,wewe kufa kitandani
Ndugu zangu nisikia,mfano tuuigeni
Tuwe tutajitolea,kwa njia yake mannani
Ili tutapojifia,pepo iwe masikani
Maswahaba wote pia,tuweni nao pembeni
Khalid na walobakia,nao tufufuliweni

Subscribe to Blog via Email

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 68 other subscribers

About Farwat Shariff

Farwata ambaye kwamba anatumia lakabu ya ashiki wa kiswahili katika uandishi wake ni kwa sasa hivi mwanafunzi wa somo la uchumi anayeishi Mombasa, Kenya. Aidha ni mjasiriamali, malenga na mwandishi wa kiswahili anayependa na aghlabu huandika kuhusu mambo yanayotokea na kuathiri jamii. Kuandika ni faraja yangu! Watu kuburudika na uandishi wangu ni furaha yangu❤

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *