MKEO KUKUPIKIA SI WAJIBU NI HISANI

      2 Comments on MKEO KUKUPIKIA SI WAJIBU NI HISANI

Nina zito la moyoni, laniumiza akili
Nalitema hadharani, basi tulieni tuli
Liwangie akilini, hasa nyie marijali
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani

Kwa kweli nasikitika, kuona yanayojiri
Mke apewa talaka, kisa hapiki vizuri
Sio sheria hakika, tumuogope qahari
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani

Na wengine wanapigwa, Kwa kuchelewa kupika
mume matusi atowa, kwa hasira na hamaka
Wanaume sio sawa, hata kwa mola rabuka
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani

Ni nani aliyesema, jikoni pa mwanamke
Tusipotoshane jama, hizo fikira tuzike
Mie leo nasimama, nasema na nisikike
mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani

Mume jikoni kungia, pia kuzikuna nazi
Tena akampikia, mke wake laazizi
Si ajabu nisikia, huyaongeza mapenzi
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani

Wasema unampenda, mke wako laazizi
Wala huezi jipinda, kumsaidia kazi
Jamani mke si punda, basi hilo tumaizi
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani

Ila mwanamke pia, basi usifure kichwa
uwe utajilalia, usiku mchana kutwa
Kuwa makini sikia, sije mumeo kavutwa
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani

Jibidiishe kupika, na usafi wa nyumbani
Nyumba itanawirika, furaha ‘tajaa ndani
Mume ‘tarudi haraka, kutoka kwake kazini
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani

Na pia kwa mola wako, ajra utaipata
Kumtwii mume wako, bila ya wewe kusita
‘tanawiri ndoa yako, utaviepuka vita
Mkeo kukupikia, si wajibu ni hisani

Subscribe to Blog via Email

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 68 other subscribers

About Farwat Shariff

Farwata ambaye kwamba anatumia lakabu ya ashiki wa kiswahili katika uandishi wake ni kwa sasa hivi mwanafunzi wa somo la uchumi anayeishi Mombasa, Kenya. Aidha ni mjasiriamali, malenga na mwandishi wa kiswahili anayependa na aghlabu huandika kuhusu mambo yanayotokea na kuathiri jamii. Kuandika ni faraja yangu! Watu kuburudika na uandishi wangu ni furaha yangu❤

2 thoughts on “MKEO KUKUPIKIA SI WAJIBU NI HISANI

 1. Hosni

  Wake vyema muelewe, Maisha kuelewana
  Mke pamwe na mumewe, Kazi kusaidiana
  Akitafuta mumewe, Mke uwalee wana
  Mmoja asilemewe, Mwingine akimuona

  Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *